Sisi sote tu watoto,tena wa baba mmoja,
kwa nini twawasha moto,kuuvuruga umoja,
enzi zile za utoto,tulicheza kwa pamoja,
Kipi kilichotusibu,watoto tunagombana?
Kama kuna ufukuto,jamani tujenge hoja,
wa upande wa mpoto,mashariki kwa pamoja,
tuiache misokoto,kwa Mungu sote ni Waja,
Kipi kilichotusibu,watoto tunagombana?
Kama jambo ni kipato,wote tunacho kimoja,
kwetu hayupo Pilato,kumsulubu mmoja,
yote haya ni mapito,kwa baba sote wamoja,
Kipi kilichotusibu,watoto tunagombana?