Monday, December 10, 2012

NARUDI NYUMBANI.

Nyumbani kweli nyumbani,ugenini ni makazi,
sana nimepatamani,kusema yote siwezi,
nyumbani kuna amani,na bora mengi malezi,
  Nataka rudi nyumbani,ugenini sipawezi.

Mambo mengi ugenini,hakika ya kilowezi,
matunda ukitamani,kupata bora huwezi,
vyakula si vya thamani,vya jokofu ndio 'pozi'
Nataka rudi nyumbani,ugenini sipawezi.

Vitu vingi vya mjini,sana vya kichokonozi,
utapopewa jibini,kiu yako haipozi,
chakula wala mezani,tena kwa kupewa kozi,
  Nataka rudi nyumbani,ugenini sipawezi.


Unapofika jikoni,kumejaa udokozi,
ukisahau sahani,kamwe kukuta huwezi,
sufuria kabatini,wameshazibeba wezi,
  Nataka rudi nyumbani,ugenini sipawezi.


Mambo ya vichochoroni,wengi wamefuzu kozi,
yanaumiza moyoni,ya wengi watu makazi,
hutowaza akilini,kama wengi 'viongozi',
  Nataka rudi nyumbani,ugenini sipawezi.

Ukifika harusini,mambo yote gozigozi
hautoingia ndani,bila kadi hauwezi
huku kwetu vijijini,jambo hilo ni la wazi
  Nataka rudi nyumbani,ugenini sipawezi.

Mahusiano mjini,wengi wetu hatuwezi,
kumejaa ufitini,vijijini hatuwezi,
usipokuwa makini,huduma kupata mwezi,
  Nataka rudi nyumbani,ugenini sipawezi.

,




.






 



 


No comments:

Post a Comment