Tu wawindaji pamoja,porini tumeingia,
sote tumejenga hoja,wanyama kujipatia,
hata sungura akija,sawa tutajigawia,
Swala tumetega wote,vipi ule peke yako?
windoni tulipotega,macho tukayapanua,
walisogolea mbega,balaa kutuletea,
tukajifunga lubega,mbali kuwafukuzia,
Swala tumetegaa wote vipi ule peke yako?
Twajua wewe mkubwa,kati yetu wawindaji,
hata kuwinda kwa mbwa,kelele utahitaji,
huwezi ruka kwa mbwa,hunacho hicho kipaji,
Swala tumetega wote,vipi ule peke yako?
Tulipoanza usasi,umoja tuliujenga,
hatukuwa na risasi,marungu tuliyatenga,
hakutokea muasi,kati kulileta janga,
Swala tumetega wote,vipi ule peke yako?
Tulijipangia zamu,kwenda kuona mitego,
tena kwa mashamushamu,tulikwenda kwa mikogo,
nasi hatukufahamu,kumbe kuna mikorogo,
Swala tumetega wote,vipi ule peke yako?
Swala alipotegeka,ilikuwa zamu yako,
begani ukamuweka,haraka chumbani kwako,
chini ukajibweteka,umezua sokomoko,
Swala tumetega wote,vipi ule peke yako?
Msiri ulomwambia,yeye hajui kuchuna,
kisu atakupatia,swala mpate kuchuna,
uchoyo umekujia,hasidi lako ni jina,
Swala tumetega wote,vipi ule peke yako?
No comments:
Post a Comment