Rais mheshimiwa,Makamu mheshimiwa
waziri mheshimiwa,naibu mheshimiwa,
spika mheshimiwa,katibu mheshimiwa,
Hili linanichanganya,nani ni mheshimiwa?
Mimi ni mkata miwa,hivi si mheshimiwa?
kutwa nakatwa na miwa,pesa kichele napewa,
na hao waheshimiwa ,kila kitu wanapewa
Hili linanichanganya,nani ni mheshimiwa?,
Hakimu mheshimiwa,wakili mheshimiwa,
wada ni mheshimiwa,afande mheshimiwa,
diwani mheshimiwa,balozi mheshimiwa,
Hili linanichanganya,nani ni mheshimiwa?
Mhudumu ofisini,siitwi mheshimiwa,
mpika chai shuleni,siitwi mheshimiwa,
msafishaji chooni,siitwi mheshimiwa,
Hili linanichanganya,nani ni mheshimiwa?
Padri mheshimiwa,Shehe ni mheshimiwa,
mbunge mheshimiwa,mjumbe mheshimiwa,
tajiri mheshimiwa,fukara alaumiwa,
Hili linanichanganya,nani ni mheshimiwa?
Mimi nalima shambani,siitwi mheshimiwa,
navuta mkokoteni,siitwi mheshimiwa,
nesi hospitalini,siitwi,mheshimiwa,
Hili linanichanganya,nani ni mheshimiwa?
Huyu mkuu wa shule,aitwa mheshimiwa,
rafiki badi Bakule,haitwi mheshimiwa,
bwana kaka kando kule,wewe ni mheshimiwa,
Hili linanichanganya,nani ni mheshimiwa?
Mgonjwa hospitali,haitwi mheshimiwa,
mwenye nzuri yake hali,haitwi mheshimiwa,
mwenye kuchunga fahali,haitwi mheshimiwa,
Hili linanichanganya,nani ni mheshimiwa?
Mambo mnayaharibu,eti ni waheshimiwa,
mnajitia mabubu,maswali mkitupiwa,
matatizo yatusibu,porojo zenu twalewa,
Hili linanichanganya,nani ni mheshimiwa?
Konisaga nashangaa,wapi tunaelekea,
neno ndugu lapotea,gizani latokomea,
hakika tulizoea,udugu liliulea,
Hili linanichanganya,nani ni mheshimiwa?
Sasa ninamalizia,neno hilo silipendi,
sana laleta udhia,latuletea makundi
usawa utapotea,sawa wa njiwa na bundi,
Hili linanichanganya,nani ni mheshimiwa?
,
No comments:
Post a Comment