Thursday, October 6, 2011

KEKI KALETA MGENI

keki sana twaipenda,sote twaipigania,
mdomoni twaisonda,na macho tunatumbua,
wengineo wanainda,yote wajichukulia,
  keki kaleta mgeni,wenyeji twagombania.

alipofika mgeni,keki ilikuwa yake,
nasi tukaitamani,japo ilikuwa kwake,
iko siku tutawini,bila tumia makeke,
  keki kaleta mgeni,wenyeji twagombania.

mgeni akaondoka,keki akatuachia,
 sasa tunafurahika,keki twaifurahia,
 vipande vikidondoka,vyote kujiokotea,
  keki kaleta mgeni,wenyeji twagombania.

keki ilikuwa moja,sasa tunaigawana
 tulikuwa ni wamoja,sasa tunafarakana
 imeuvunja umoja,mapanga tunakatana,
  keki kaleta mgeni,wenyeji twagombania.

 keki yao sio safi,kama zetu za asili,
 keki yao kama fifi,katu hutamani huli,
 ni nyepesi kama sufi,keki hiyo mimi sili
  keki kaleta mgeni,wenyeji twagombania.

 keki imeleta vita,wote imetugawanya,
 kusema mi sitasita,nimepata huu mwanya,
 beti zikifika sita,ujumbe waweza penya,
  keki kaleta mgeni,wenyeji twagombania.

amerudi kwa ujanja,na keki nyingine tena,
udugu tumeuvunja,kutwa kucha twagombana,
keki hizo tumeonja,sasa tunafarakana,
  keki kaleta mgeni,wenyeji twagombania.

keki zao kumbe chungu,tulidhania ni tamu,
 nasema haki ya Mungu,imeshaniisha hamu,
 sitaki nyumbani kwangu,keki hizo kweli ngumu,
  keki kaleta mgeni,wenyeji twagombania
.
 kila mtu atamani,keki achukue yote,
 utu hauna thamani,wokovu tukaupate,
 keki za kihayawani,hadi vichwa watukate,
  keki kaleta mgeni,wenyeji twagombania.

chukueni keki zenu,kwanza zaleta majanga,
 hebu rudisheni kwenu,tumevichoka visanga,
 keki zenu ni za kwenu,sasa tumepata mwanga,
  keki kaleta mgeni,wenyeji twagombania.

No comments:

Post a Comment