Thursday, September 29, 2011

PETE

pete kitu cha ajabu,kwangu inaleta adha,
zipo pete za dhahabu,na pia zile za fedha,
avaa kaka Twalibu,na pia dada Faidha,
  nani aivae pete,na nani asiivae?.

mimi nilifikiria,pete ni za wana ndoa,
kidole cha kuvalia,cha pete sote twakijua,
lakini ninashangaa,sipo wanapovalia,
  hakika sijaelewa,nini maana ya pete.


kama ni ya wana ndoa,mbona wengi wanavua,
nini wanadhamiria,vidoleni waitoa,
jibu kweli sijajua,wao watatupatia,
  jamani sijaelewa,wapi pa kuvaa pete.

kama ni uaminifu,mbona wengi wazinifu,
wajitia watiifu,na mioyo mikunjufu,
tabia zao zakifu,zatia kichefuchefu,
  hizo pete mnavaa,sijui maana yake.

hata kwenye maandiko,kule kwenye biblia,
ukienda soma huko,mengi utajipatia,
utapata muamko,maana utaijua,
  yule mwana mpotevu,ndiye alivishwa pete.

ndoa sio upotevu,sisi tuvae za nini,
kama ni uvumilivu,hilo latoka moyoni,
yataka ustamilivu,uweze kuibaini,
pete nivae ya nini,sijui maana yake.

hata wanaozivaa,mambo yao ya kihuni,
wale wanaozivua,tabia utabaini,
bora asiyeivaa,akamtii Manani,
  ukweli hutobaini,kuhusu pete ya ndoa.

wengi wanaziabudu,'mipete'vidole vyote,
haya mambo ya ajabu,utayaona popote,
'mipete'sio thawabu,hilo jambo kweli tete,
  'mipete' vidole vyote,inaashiria nini?

kwa maumbo zipo nyingi,nyingine zinachukiza,
masonara wako wengi,urembo kuziongeza,
maswali zazua mengi,vigumu kujieleza,
  pete mfano wa chura,mnazivaa za nini?

angalia vidoleni,'mipete ni ya ajabu,
mna nini fikrani,kwangu sioni sababu,
kwangu sawa na majini,sitaweza zijaribu,
pete ya ndoa unayo,nyingine za kazi gani?

nyingine zatoka wapi,maumbo siyo bayana,
 hata kama mmekopi,za ndoa zitofanana,
 hivi hamziogopi,enyi wana wa Rabana,
   vaeni hiyo 'mipete',mseme maana yake.

 hayo ni mawazo yangu,japo yatia uchungu,
 pete sitovaa kwangu,wala familia yangu,
 hata mnifunge pingu,sitaki kidole changu
   Yule mwana mpotevu,ndiye alivikwa pete.

No comments:

Post a Comment