Wednesday, February 13, 2013

NDEGE IMESHAONDOKA

Wengi twapenda tembea,maeneo mbalimbali,
wazo linapokujia,tena kama una hali,
utakachofikiria,kwenda popote mahali,
  Ndege imeshaondoka,kata tiketi nyingine.

Ndege ulotegemea,sasa imefika mbali,
kwako kilichobakia,hali yako ni muhali,
punguza kufikiria,endelea saka mali,
  Ndege imeshaondoka,kata tiketi nyingine


ndege uliyozoea,imekuwa bei kali,
siti ulizokalia,kwako sasa bei ghali,
zile nilikukatia,kwako tena si halali,
  Ndege imeshaondoka,kata tiketi nyingine.

Kote tulikotembea,hata visiwa vya Bali,
uliona mazoea,gharama hukuzijali,
kutwa ulijidekea,kumshinda hata mwali,
  Ndege imeshaondoka,kata tiketi nyingine.

Jinsi nilikutendea,mimi wa Mungu mjoli,
uliona mchekea,ukajifanya mkali,
tiketi kunitupia,kusema si mali kitu,
  Ndege imeshaondoka,kata tiketi nyingine.

Hata basi safiria,hiyo ndiyo yako mali,
ndege acha fikiria,kwa yake hayo makali,
yasahau mazoea,sasa nakupa ukweli,
  Ndege imeshaondoka,kata tiketi nyingine.

Mangapi nitongea,hayabadili ukweli,
kutwa nikisimulia,ukweli sitabadili,
kitu kilichobakia,vumilia kama soli,
Ndege imeshaondoka,kata tiketi nyingine.

Vipi nikihadithia,sitabadili ukweli,
machozi nikiyatoa,sitobadili kauli,
wengi watanishangaa,jitu hili ni katili,
Ndege imeshaondoka,kata tiketi nyingine.

mimi nilifikiria,una pungufu nauli,
kumbe mi nilichelea,huna hata ya ugali,
kama mboga yapelea,ongeza na pilipili,
  Ndege imeshaondoka,kata tiketi nyingine.

Ushauri ninatoa,uspunguze kusali,
nauli kujipatia, walau basi la pili,
ushauri zingatia pia muombe Jalali,
  Ndege imeshaondoka,kata tiketi nyingine.


















NI KWELI WATAKA KAZI?

Tunapotafuta kazi,heshima tunaonyesha,
kwamba tumepata kozi,na vyeti kuvionesha,
vyeti vyetu si vya wizi,hili tunadhihirisha
  Ni kweli wataka kazi au wataka kingine?

Ulishindia viazi,kutwa kucha ulikesha,
hukufanya upuuzi,muda wako ulitosha,
hayo uliyamaizi,wazembe walikupisha,
Ni kweli wataka kazi au wataka kingine?

Sasa umepata kazi,umeanza kutuchosha,
umeanza udowezi,hivi sasa nakupasha,
kwa bosi mchokonozi,tamaa inakuwasha,
Ni kweli wataka kazi au wataka kingine?

Wewe ni msaidizi,vyombo kwetu unaosha,
wapi ulipata kozi,waanza tugombanisha,
tuko kama wakimbizi,chuki twajibebanisha,
Ni kweli wataka kazi au wataka kingine?

Sasa tumekuwa nazi,vichwa watugonganisha,
hivi tumejua wazi,umbea unakuwasha,
huyawezi maamuzi,kila jambo wapotosha,
  Ni kweli wataka kazi au wataka kingine?

wewe ni kama mkwezi,majungu kuyapandisha,
kazi yako upakuzi,fitina kufurumusha,
hauishi uchakuzi,tabia yako yatisha,
  Ni kweli wataka kazi au wataka kingine?

Kazi wewe hauwezi,sote tumebainisha,
fitina ni muenezi,cheo unajipand isha,
sasa muombe mwenyezi, mbinguni kukufikisha,
Ni kweli wataka kazi au wataka kingine?

Tabia kama ya mbuzi,mapembe umepandisha,
mabawa kama nyambizi,nani akupe motisha,
acha wako upekuzi,ziwani tutakurusha,
Ni kweli wataka kazi au wataka kingine?

Kusema yote siwezi,nimekwisha kujulisha,
nakwambia simalizi,beti nyingi zinatosha,
usipatwe jinamizi,nani ataja lishusha,
Ni kweli wataka kazi au wataka kingine?

Mimi si king'ang'anizi,polepole najishusha,
sijatoa simulizi,ya moyoni nimeshusha,
nimekwisha kubarizi,kazi nakupa Elisha,
  Ni kweli wataka kazi au wataka kingine?


Konisaga Mwafongo 0717248828










UCHUNGUZI UNAENDELEA

Washairi nauliza,jibu nipeni yakini,
swali limeniumiza,jibu sijalibaini,
uchunguzi wanikwaza,jibu waweka sirini,
   Hivi huo uchunguzi,majibu mwatupa lini?

Soko lilipoungua,mengi mlitueleza,
kamanda aelezea,chanzo bado chatatiza,
sisi tunasubiria,wao nini wanawaza,
Hivi huo uchunguzi,majibu mwatupa lini?

Jambazi amekamatwa,vyombo vyote mwatangaza,
hakika alipopatwa,sana tulijiliwaza,
hakuna aliyesutwa,sasa twaona mwangaza,
Hivi huo uchunguzi,majibu mwatupa lini?

Wizi wa mali ya umma,mwauripoti kwa kina,
utadhani huko nyuma,hamkupata uona,
magazeti tunasoma,runingani tunaona,
  Hivi huo uchunguzi,majibu mwatupa lini?

kakamatwa muuaji,aliyewaua wengi,
mambo mengi hamtaji,aliuza hata bangi,
aliuvuruga mji,sasa miji hatafungi,
  Hivi huo uchunguzi,majibu mwatupa lini?

wanaotupa vichanga,wahitaji uchunguzi?
tunaowaita wanga,ni wa nini uchunguzi,
porojo mnazipanga huo sasa upuuzi,
  Hivi huo uchunguzi,majibu mwatupa lini?

Tairi limepasuka,ajali ikatokea,
hakuna aliyesuka,limekuwa kama baa,
mioyo inashituka,maisha yanapotea,
Hivi huo uchunguzi,majibu mwatupa lini?

Huo wenu uchunguzi,mimi ninauchukia,
unatupa usingizi,kwa tunavyosubiria,
imekuwa upuuzi,nini kinaendelea,
  Hivi huo uchunguzi,majibu mwatupa lini?

Mimi sijapata soma,majibu ya uchunguzi,
labda  mliosoma,mwaniona mchochezi,
sasa nasimama hima,mimi si mchokonozi,
Hivi huo uchunguzi,majibu mwatupa lini?

Namaliza kwa kusema,uchunguzi endelea,
umeshachoka kusoma,uchunguzi  fatilia,
hapa mimi ninakoma,hivi sasa nasinzia,
Hivi huo uchunguzi,majibu mwatupa lini?
Konisaga Mwafongo 0717248828