Tuesday, May 28, 2013

NENO "KAMA" LACHANGANYA


NENO “KAMA”LACHANGANYA.
Neno “kama” kweli  gumu,kulitumia vigumu,
Kama wasoma isimu,tupunguzie ugumu,
Lugha si mwanaharamu,nayo inayo rasimu,
  Neno “kama”lachanganya,jamani tuwe makini.

Mimi “kama’ ni mwalimu,wiki hii niko zamu,
Nikikukuta sehemu,usije kunilaumu,
Mwalimu ulihitimu,”kama”hapo si sehemu,
    Neno “kama”lachanganya,jamani tuwe makini

Mheshimiwa hakimu,kazi yako kweli ngumu,
Unaposoma hukumu,roho kweli iwe ngumu,
Na mimi “kama” hakimu,mvua sita kazi ngumu,
  Neno “kama”lachanganya,jamani tuwe makini 

Mimi “kama”mhudumu,faili zamu kwa zamu,
Wote muwe na nidhamu,nisjie panda wazimu,
Kazi yangu mfahamu,ni ngumu msilaumu,
  Neno “kama”lachanganya,jamani tuwe makini

N a mimi “kama”Adamu,nimemzaa Swaumu,
Mtoto wangu wa damu,Mola amenirehemu,
Nitampenda dawamu,kama mwana wa Kikwemu,
  Neno “kama”lachanganya,jamani tuwe makini

Mbunge wetu udumu,hii ni yako awamu,
Watu wako tuna hamu,tatua kero kwa zamu,
Na mimi “kama”mwalimu,kusema siishi hamu,
  Neno “kama” kwa hakika,hapo  ni mahala pake.

Viongozi silaumu,neon hilo kwenu gumu,
Mwatushushia “mabomu”,najua hamfahamu,
Mbona mkijaza fomu,huwa mnalifahamu,
    Neno “kama”lachanganya,jamani tuwe makini  

Naweka chini kalamu,neno “kama”lifahamu,
Sio kuwa nashutumu,neno “kama”sina hamu,
Ninawaomba walimu ,lirudisheni utamu,
     Neno “kama”lachanganya,jamani tuwe makini
Konisaga Mwafongo
Simu:0717  24 88 28

No comments:

Post a Comment