Tuesday, November 5, 2013

RAFIKI HUTOMJUA



Kupata mwema rafiki,sala yapasa shiriki,
Wako wengi wanafiki,tena vinara wa chuki,
Jaribu kumhakiki,Mola akupe a haki,
  Rafiki hutomjua,asilani abadani.

Rafiki mfano nyuki,utaishia mikuki,
Atakujaliza dhiki,na kukujaza mikiki,
Hutoipata riziki,kwa rafiki alo “shirki”,
    Rafiki hutomjua,asilani abadani.

Wengi wao wazandiki,shida hawatoshiriki,
Misibani hawatoki,kukung’ong’a watabaki,
Utabaki kuhamaki,furaha hutomiliki,
    Rafiki hutomjua,asilani abadani


Konisaga  Mwafongo-0717 248828/0767 24 88 28 Mbeya.

TUMEPOTEA



Nyuma nikiangalia,hakika tumepotea,
Mbele nikiangalia,jua lazidi kuchwea,
Twapoteza asilia,vya wageni twapokea,
    Sio kila cha mgeni,yatupasa kupokea.

Ngoma za kiasilia,hebu sasa angalia,
Haziwezi kuvutia,walisha tuharibia,
Midundo tulosifia,sasa ni historia,
Sio kila cha mgeni,yatupasa kupokea.

Ukarimu angalia,sivyo tulivyozoea,
Usasa umetukaa,ubize twasingizia,
Udugu “ulishapaa”,tumebaki kuduwaa,
Sio kila cha mgeni,yatupasa kupokea.

Kwa jirani kutembea,sasa waitwa umbea,
Wataka hali Julia,eti unawasumbua,
Simu ungewapigia,mbona wangeipokea,
Sio kila cha mgeni,yatupasa kupokea.

Mola ametujalia,mlo wetu asilia,
Sasa kilichoingia,hakika waweza lia,
Makapi watupatia,uleo wasingizia,
Sio kila cha mgeni,yatupasa kupokea.

Gharama twajiletea,mazishini angalia,
Mapesa tunayatoa,na sare kuandalia,
Tungeweza kujitoa,uhai hangaikia,
Sio kila cha mgeni,yatupasa kupokea.

SHAIRI GUMU LA NINI?



Mashairi burudani,pale unapoyasoma,
Shairi gumu la nini,ni nini unachopima,
Halikai akilini,kando utalisukuma,
  Shairi gumu la nini,halileti burudani.

Yasome magazetini,kweli kichwa kitauma,
Unaweza ukadhani,kaandika kisukuma,
Kama si cha upareni,basi lugha ya Musoma,
  Shairi gumu la nini,halileti burudani.

Ufikapo vibandani,gazeti ukalifuma,
Utafurahi moyoni,na tena utajituma,
Pesa ipo mfukoni,nyumbani nitalisoma,
  Shairi gumu la nini,halileti burudani.

Soma kilichomo ndani,shairi hutolisoma,
Wajigeuza kitini,kweli leo unakoma,
Sio tena burudani,masikio yanavuma,
  Shairi gumu la nini,halileti burudani.

Mashairi kweli fani,wengi twapenda yasoma,
Washairi andikeni,tutayoweza kusoma,
Unamkomoa nani,Konisaga ninasema,
  Shairi gumu la nini,halileti burudani.

Konisaga  Mwafongo-Mbeya  0717 24 88 28/0767 24 88 28