Tuesday, November 5, 2013

TUMEPOTEA



Nyuma nikiangalia,hakika tumepotea,
Mbele nikiangalia,jua lazidi kuchwea,
Twapoteza asilia,vya wageni twapokea,
    Sio kila cha mgeni,yatupasa kupokea.

Ngoma za kiasilia,hebu sasa angalia,
Haziwezi kuvutia,walisha tuharibia,
Midundo tulosifia,sasa ni historia,
Sio kila cha mgeni,yatupasa kupokea.

Ukarimu angalia,sivyo tulivyozoea,
Usasa umetukaa,ubize twasingizia,
Udugu “ulishapaa”,tumebaki kuduwaa,
Sio kila cha mgeni,yatupasa kupokea.

Kwa jirani kutembea,sasa waitwa umbea,
Wataka hali Julia,eti unawasumbua,
Simu ungewapigia,mbona wangeipokea,
Sio kila cha mgeni,yatupasa kupokea.

Mola ametujalia,mlo wetu asilia,
Sasa kilichoingia,hakika waweza lia,
Makapi watupatia,uleo wasingizia,
Sio kila cha mgeni,yatupasa kupokea.

Gharama twajiletea,mazishini angalia,
Mapesa tunayatoa,na sare kuandalia,
Tungeweza kujitoa,uhai hangaikia,
Sio kila cha mgeni,yatupasa kupokea.

No comments:

Post a Comment