Thursday, September 1, 2011

HATA MIMI NASHANGAA.

Jinsi unavyoshangaa,hata mimi nashangaa,
jambo lililotokea,kweli ni kizaaza,
sitoweza vumilia,kichwa kipate tulia,
 Hata mimi nashangaa,jinsi unavyoshangaa

Habari ilozagaa,akili bado tulia,
eti mtoto kuzaa,na baba alomzaa,
kamwe mi sitotulia,sipati huo wasaa,
  Hata mimi nashangaa,jinsi unavyoshangaa.

Mama binti wagombea,'kabuzi'kalobobea,
mimacho wametumbua,kijana wagombania,
wote ni viruka njia,ukimwi jitafutia,
  Hata mimi nashangaa,jinsi unavyoshangaa

Mwalimu na mwanafunzi,eti nao ni wapenzi,
haya ni gani mafunzi,huu kwetu ni ushenzi,
natamani piga konzi,au kibao cha banzi,
 Hata mimi nashangaa,jinsi unavyoshangaa.

Baba na mtoto wako,mnachangia kimada,
ninyi sawa mbwa koko,kuzurura kwake ada,
kama ni wali ukoko,hamfai kwenye eda,
  Hata mimi nashangaa,jinsi unavyoshangaa.

Dakitari wanichosha,mgonjwa wamtamani,
nani alikufundisha,sijaona asilani,
badala kumponesha,mapenzi wamtamani,
  Hata mimi nashangaa,jinsi unavyoshangaa.

Wewe bosi ofisini,hakika watia fora,
umuonapo karani,moyoni wapiga kura,
fikiria akilini,uhai ni kitu bora,
  Hata mimi nashangaa jinsi unavyoshangaa.

Ewe kabinti kadogo,uhai kwako ni mali,
watembea kwa mikogo,kupita kila mahali,
kwa rika bado mdogo,bado kukua akili,
  Hata mimi nashangaa,jinsi unavyoshangaa.

Na viongozi wa dini,pepo huyo awatoke,
mwatamani waumini,mwalizua sekeseke,
hili utalibaini waulize wanawake,
  Hata mimi nashangaa,jinsi unavyoshangaa.

Nani aliyebakia,MOLA akajivunia,
utukufu tumevua,tumevaa magunia,
wangapi wamesalia,Mungu kuwahurumia,
  Hata mimi nashangaa,jinsi unavyoshangaa..
,





No comments:

Post a Comment