Tuesday, September 20, 2011

ASHA

nimemuona mtoto,kwa jina aitwa Asha,
siyasemi kwa mkato,hakika ninakupasha,
mapigo yapamba moto,lini nitawasilisha,
Jinsi alivyo mzuri,mfanowe sijaona.

kila akitabasamu,macho yake ya bashasha,
katu haiishi hamu,kumtazama si chosha,
kwa kutumia kalamu,sifa zake nitarusha,
hakika ni mtulivu,mtoto aitwa Asha.

Asha ulivyoumbika nani asiyekubali,
mwili ulivyopangika,kila nguo yakubali
wanaume twageuka Mola alivyokujali
watu wote tunawaza nani tampata Asha.

pale ukitabasamu,mwiliwaishiwa nguvu,
nabaki kama sanamu,moyoni ninalo kovu,
pokea japo salamu,unitoe maumivu
asha ninavyokupenda,moyoni hilo wajua

wengi wanakusumbua,kila siku wakufata,
hilo ninalitambua.wote wacheza karata,
kwani ushaangalia,nani kiu atakata,
kukwambia nakwambia,moyo kwako umetua.

pale unapoongea,waongea kwa upole,
nataka kusogelea,nishike japo vidole,
busu nipate tupia,likuchome kama mwale,
kama neno nakupenda,hilo ulishazoea.

mwendo wako taratibu,sana unakupendeza,
wajivuta kwa adabu,nani atayekubeza,
mimi naona sababu sasa nakubembeleza
beti hizo kazi kwako,naomba tuwe pamoja

tena naiangalia,ngozi yako iking'ara,
jinsi ilivyotulia,haina hata harara,
kweli nakusimulia kwa upole si papara,
hakika ninakupenda lugha umeizoea

ngozi yako ni nyororo,laini kama hariri,
sijaona mgogoro,naipenda kwa hiyari,
hutaona hata Moro,nenda hata Ikwiriri,
ngozi bila vipodozi hakika unapendeza.

sauti yako makini,nyoka atoka pangoni,
nimepima kwa makini tafakuri akilini,
nikitazama usoni,ninakupenda mwandani,
wazo najua unalo ni lipi linakutesa

sasa naomba wasaa,baada ya kazi yako,
ninataka nikwambie likae moyoni mwako,
uzito kulipatia,nipate kuwa mwenzako
nini kilichobakia,nimeweka yote wazi,

tukiwa wote nyumbani,nyumba utapendezesha,
utapokuwa jikoni,chakula kuharakisha,
ukifika sebuleni,karibisho kwa bashasha,
wewe ua la nyumbani,karibu nyumbani kwangu

ua nitaweka wapi,sitaliweka juani,
ua sio kama pipi,zinazouzwa dukani,
ua hilo kwa kifupi si kuweka barazani,
ua ninaloongea,hakika ni wewe Asha.

wimbo gani nikwimbie,yote yamejieleza,
lugha gani nikwambie,upate jipeleleza,
shairi nikutungie lipate  kukuliwaza,
vyote unavielewa,jibulo litanipoza

sasa chukua kalamu,jaribu andika kitu,
hata kama kwa awamu,si sawa kuacha katu,
kwa  wako utaalamu,utaupenya msitu,
mapenzi sawa msitu,kamanda utaupenya

kama sio kwa shairi,tumia japo kauli,
moyoni itoe siri,iweke kwangu mahali,
jibu nishalikariri,nitoe kwenye muhali
nipe japo taabasamu,liwe ndio jibu lako

mashairi yapo mengi siwezi kuyamaliza
sifa zako zipo nyingi,ngapi nitakueleza,
na vikwazo vipo vingi,najua hutoteleza
gari langu liko wazi na abiiria ni wewe.

sasa ninatua hapa,kuandika kwangu jadi,
kama ni nguvu za papa,karata lasti kadi,
naishia hapahapa,kwako naipiga hodi
hodi nilishaipiga nasubiri kuingia.

No comments:

Post a Comment