Tuesday, September 20, 2011

HIYO SIO MALI YAKO

imenibidi kutunga,kueleza kero hii,
mdomo sitaufunga,naeleza wasanii,
mtasema ninachonga,masimango sisikii,
Hiyo sio mali yako,katu usiichukue.

waingia ofisini,kwa adabu na heshima,
unajitupa kitini,kwa uso wenye huruma,
jicho lako kabatini,kitu umeshakifuma,
Hiyo sio mali yako,katu usiichukue.

ukikutacho mezani,kina makusudi yake,
 sikukiweka uani,kinalo jukumu lake,
 wakitia mfukoni,nabaki na sekeseke,
Hiyo sio mali yako,katu usiichukue.

ukiisha ichukua,nabaki nawayawaya,
 naanza kuangalia,yaweje jamani haya,
 hasara niloingia,imeshanitia haya,
Hiyo sio mali yako,katu usiichukue
.
naongea kwa uchungu,mwili unatetemeka,
 katu sitaki majungu,ukweli nitauweka,
ukija ofisi yangu,kwanza staarabika,
Hiyo sio mali yako,katu usiichukue.

magazeti na vitabu,vyote wajichukulia,
imeisha kuwa tabu,majonzi unanitia,
ungeeleza sababu,vyote ningekupatia
Hiyo sio mali yako,katu usiichukue
.
hatuwezi piga yowe,kukuita wewe mwizi
unajijua mwenyewe,ziache tabia hizi,
utalili mkwewe,punde tutakumaizi
Hiyo sio mali yako,katu usiichukue.

No comments:

Post a Comment