Tuesday, September 6, 2011

KARAMU TUNAZIPENDA

wengi twapenda karamu,twazisubiri kwa hamu,
kama hili hufahamu,jibu utapata humu,
utavipata vitamu,kamwe hutapata sumu,
  karamu tunazipenda,nyingi zake si sahihi

nilichukua kalamu,kueleza umuhimu,
ninataka kufahamu,japo katika awamu,
karamu sio swaumu,kupata si jambo gumu,.
  karamu tunazipenda,nyingi zake si sahihi

karamu nyingi fahamu,zaweza kuleta pumu,
jinsi tunavyozifomu,nyingizo sio muhimu
kuzijua nina hamu,moyo pate tabasamu
  karamu tunazipenda,nyingi zake si sahihi

mimi ninavyofahamu,karamu si marhamu,
imeshaniisha hamu,nitamwuliza mwalimu,
vipi  hizo zinadumu,tena daima dawamu,
  karamu tunazipenda,nyingi zake si sahihi

unajilipua bomu,tena huku wafahamu,
hiyo kwako ni karamu,kweli huna ufahamu,
ulitumia vidumu,kuliunda hilo bomu,
  karamu tunazipenda,nyingi zake si sahihi

wanipatia salamu,moyoni huna fahamu,
waanza kumwaga sumu,ofisini nisidumu,
umekuwa ni hasimu,kama unavuta'ndumu'
  karamu tunazipenda,nyingi zake si sahihi

ndoa yangu haidumu,unajifanya hakimu,
asubuhi wajihimu,unaleta uhasimu,
kwetu wewe si Rahimu,ndoa yetu itadumu,
  karamu tunazipenda,nyingi zake si sahihi

ninapenda ufahamu,sitaki ugomvi humu,
wapi ulikohitimu,feki wako ualimu,
unatushusha stimu,nenda zako jehanamu
  karamu tunazipenda,nyingi zake si sahihi

No comments:

Post a Comment