mimi bado ni mdogo,swali siwezi kujibu,
swali halina udogo,kupata lake jawabu,
huyu babetu mdogo,wote kwetu ni ajabu,
bado hakika sinayo,huyu ndiye baba yetu.
nimeona baba wengi,tena na zao busara,
wenye watoto kwa wingi,hata kama ni fukara,
upendo kwao ni mwingi,uliojaa tijara,
bado hakika sinayo,huyu ndiye baba yetu.
baba ananishangaza,kweli hana shukrani,
kutwa anajitangaza,eti anatuthamini,
kazi yake kujikweza,eti yeye wa thamani,
bado hakika sinayo,huyu ndiye baba yetu.
kama angekuwa wetu,asingekuwa muoga,
kama tatizo ni letu,angesema bila woga,
angetupa haki yetu,watoto sio mizoga,
bado hakika sinayo,huyu ndiye baba yetu.
mama yetu hatunaye,jibu angetupatia,
baba ambaye tunaye,mashaka twamtilia,
hivi kweli ndiye yeye,jirani twaulizia,
bado hakika sinayo,huyu ndiye baba yetu.
No comments:
Post a Comment