hakika inachukiza,ukorofi ukianza,
tena inaleta kiza,mtu manza akianza,
na pia inatatiza,vurugu inapoanza,
mtu akikukosea,jitahidi msamehe.
wengi wananishangaza,pindi wanapochukia,
huanza na kutangaza,wanashindwa kutulia,
hasira wanazijaza,busara yatokomea,
mtu akikukosea,jitahidi msamehe.
mtu anapokukosa,ni budi mfikiria,
hekima ukiikosa,hasira itatopea,
huruma utaikosa,mbumbumbu utabakia,
mtu akikukosea,jitahidi msamehe.
mimi sana nashangaa,ugomvi unapoanza,
chanzo ukifikiria,sababu zipate kwanza,
sio mambo kurukia,utakuja kujiponza,
mtu akikukosea,jitahidi msamehe.
ugomvi kitu kibaya,mimi ninakichukia,
tena unatia haya,nikianza simulia,
mambo haya ni mabaya,sipendi yakitokea,
mtu akikukosea,jitahidi msamehe.
kama wewe umekosa,kamuombe samahani,
usimuwekee visa,hasira hutaiwini,
usivifunge vitasa,vya sanduku la amani,
mtu akikukosea,jitahidi msamehe.
kusamehe kazi ngumu,usipo muomba Mungu,
ukipata jambo gumu,kufikiri ni muhimu,
usifanye kichwa ngumu,msamaha walazimu,
mtu akikukosea,jitahidi msamehe.
No comments:
Post a Comment