Tuesday, September 6, 2011

KILA KITU KINA JINA

kila mtu ana jina,hata kama yafanana,
kila kitu kina jina,kuweka vitu bayana,
kila mnyama kwa jina,hata kama wafanana,
  kila kitu kina jina,kuweka mambo bayana.

mi sijapata kuona,kitu kisicho na jina,
mitindo nguo twashona,yote yapewa majina,
magari unayaona,ya starehe mwanana,
  kila kitu kina jina,kuweka mambo bayana.

hata kama twafanana,tabia zitofanana,
nyuso zetu zote pana,kweli twafanana sana,
yachunguze kwa mapana,yote ajua Rabana,
  kila kitu kina jina,kuweka mambo bayana.

majina tunapeana,mwingine aitwa Ana,
majina si kufaana,hilo halina maana,
jina baya mi nakana,nipate janga kupona, 
  kila kitu kina jina,kuweka mambo bayana.

wewe Vumi msichana,yeye Juma mvulana,
nywele vipi mwasukana,jinsia mmepishana,
saluni mwasukumana,tabia hiyo nakana,
  kila kitu kina jina,kuweka mambo bayana.
wavulana wapeana,vitu kama wasichana,
sketi zinawabana,huku wao wavulana,
watembea kisichana,kwapani pochi wabana,
  kila kitu kina jina,kuweka mambo bayana.
tukuite lipi jina,tabia zimepishana,
jinsi tunavyokuona,umbo lako si bayana,
sauti unaibana,mwendo wako kisichana,
  kila kitu kina jina,kuweka mambo bayana.

Mola hayo anaona,siku moja takutana,
heleni zivojishona,pete nazo kila kona,
kinyaa mimi naona,kila siku na sonona,
  kila kitu kina jina,kuweka mambo bayana.

No comments:

Post a Comment