Tuesday, September 6, 2011

CHETI CHA NDOA.

Vyeti vyote twavijua,toka vyuo mbalimbali,
hata ukivichungua,hakika utakubali,
jambo ninaloshangaa,vyeti vingi si vya kweli,
  Cheti hiki unapewa,bila ya kwenda chuoni.

Cheti hiki mnatoa,sijaona diploma,
wasomi nawashangaa,mwakipokea kwa dhima,
tena mwakichekelea,kwa heshima taadhima,
   wewe una digrii,cheti wapata cha nini

wapi niliposomea,mnanipatia cheti,
sana hili nashangaa,hoja namwaga kwa beti,
cheti mnanipatia,kweli kitaleta shoti,
    Cheti bila mtihani,sijaona asilani.

hata kusoma sijui,ninakariri majibu,
fumbo hili halifai,mengi yataja nisibu,
siri ya ndani hujui,ni nini chakughiribu,
   majibu tunakariri,watu wanashangilia

nimempenda Mwasiti,ndoa tunaitangaza,
shehe aja anaketi,aanza kuwauliza,
jama kipo kizuizi,watu hawa nawaoza,
  Chuo gani tulikwenda,mnatupatia cheti.

Koni wampenda pendo,ndio baba Askofu,
sasa tunaanza mwendo,mambo yetu manyoofu,
kila mtu ana windo,na mioyo mikunjufu,
  mchezo wa kuigiza,cheti hicho unapewa

chuo cha ndoa ki wapi,mimi nipate somea,
majibu wote twakopi,cheti bila kusomea,
vyeti hivyo kama pipi,sisi mnatugawia,
cheti hicho sikitaki,sana chaleta majuto.

kichekesho maprofesa,nao wanakipokea,
ni wapi walipodesa,chuo walikopitia,
ujinga unawatesa,mkumbo watumbukia,
  wasomi wanapata cheti,bila kusoma chuoni.

wengine mbio bomani,ndoa kwenda ifungia,
nayo katu sitamani,balaa najizulia,
cheti bila ya chuoni,uchuro twajizolea,
  wote wenye vyote hivyo,hakika nawashangaa.

kashangae kanisani,nderemo vigelegele,
wachumba wanasaini,mwanzo wa ngoma ni lele,
sijaona maishani,kitu mfano wa kile,
  usinishangae mimi,kashangae hicho cheti.

viwango hawatakidhi,vyeti hivyo ni balaa,
jinsi vinavyoniudhi,wengine wajivunia,
vyeti hivyo ni maradhi,ya moyo jitafutia,
  hicho kinaitwa cheti,diploma iko wapi

kama hujajiuliza,hebu anza jishangaa,
si kwamba nakipuuza,heshima nakitunzia,
sifa tulivyokijaza,watu wakifukuzia,
  sote twakijua cheti,digrii iko wapi?

najua nitawakwaza,maoni yangu kutoa,
hebu jaribu kuwaza,chuo gani wanatoa,
cheti sitakipuuza,wote  mmekiridhia,
  dole gumba linatosha,kupata cheti cha ndoa.

kakague vyeti vyote,saini yako hukuti,
kwenye mikataba yote,kuwepo hiyo shuruti,
vyeti vya ndoa kalete,havielezi wakati,
  jambo hili lichunguze,vyeti vingi tunafoji.

beti nyingi zinachosha,wengi zinawachukiza,
katu siwezi jikosha,sipendi kuwachokoza,
beti nilizozishusha,sio lengo kuwakwaza,
  kama wakijua chuo,niambie nikasome.























 wote
















No comments:

Post a Comment