hakika wajidanganya,ukidhani ni mwezio,
urafiki mlifanya,tena kwa mafanikio,
akili hukuikanya,tena kwa mfatilio,
Ulidhani unajua,kumbe unajidanganya.
shule mlisoma wote,na tena darasa moja,
mliongozana kote,tena kwa ule umoja,
mpira kucheza nyote,mlikuwa halimoja,
Ulidhani unajua,kumbe unajidanganya.
mtaa wenu mmoja,tena kuitana ndugu,
sisi mnazimmoja,na yeye kwao ni Pugu,
jambo tulilolingoja,sasa imekuwa pwagu,
Ulidhani unajua,kumbe unajidanganya.
wakumbuke marafiki,mlipokuwa watoto,
hamkuwa wanafiki,mambo kufanya mkato,
hata nawe wasadiki,mambo yote motomoto,
Ulidhani unajua,kumbe unajidanganya.
leo hii mmekua,mnapigiana simu,
ahadi mwajipangia,kila mtu ana hamu,
barua wamwandikia,tena huna urasimu,
Ulidhani unajua,kumbe unajidanganya.
mkomba yuko Kahama,na wewe una hakika,
atakwambia kahama,anazo nyingi pilika,
kumbe huko amekwama,kimaisha kapigika,
Ulidhani unajua,kumbe unajidanganya.
unampigia Ali,rafiki yako kipenzi,
ukamlilie hali,unazikumbuka enzi,
Ali sasa hakujali,wamghasi kama nzi,
Ulidhani unajua,kumbe unajidanganya.
No comments:
Post a Comment