Thursday, September 15, 2011

LEA WATOTO VIZURI

Mungu amewabariki,uzao kuwapatia,
kupata wana riziki,ni mola akijalia,
haihitaji mikiki,Mola ndiye anatoa,
  Lea watoto vizuri,kuwatesa ni laana.

wengi wanahangaika,kwenda hata kwa waganga,
kwingi wanazunguuka,wafika hata ulanga,
wanazidi kuzuzuka,hata wajifunza wanga,
  Lea watoto vizuri,kuwatesa ni laana.

mara nyingi nashangaa,wengi watupa watoto,
huruma inatujaa,haya ni gani mapito,
 watoto tunaozaa,ubora zaidi vito,
  Lea watoto vizuri,kuwatesa ni laana.

wengineo washangaza,watoto wingi wa timu,
 kwa watu wajitangaza,kuzaa kwao si zamu,
 nguo zao zaongoza,viraka zamu kwa zamu,
  Lea watoto vizuri,kuwatesa ni laana.
kama chakula wapate,kingi cha kutosheleza,
asubuhi kwa mkate,hata kwa wali na pweza,
matunda ukayapate,afya zao utakuza
  Lea watoto vizuri,kuwatesa ni laana.

No comments:

Post a Comment