Tuesday, September 20, 2011

SAFARI

safari niliyoanza,Mola ndiye anajua,
nilifikiria kwanza,jibu sikulipatia,
maisha mapya kuanza,yakupasa fikiria,
  Maisha kuwa na mwenza,Mola naomba jalia.

siku nyingi niliwaza,atakuwa jinsi gani,
asiwe wa kujikweza,na kuleta tafrani,
awe kujinyenyekeza,siku zote kwa Manani.
Maisha kuwa na mwenza,Mola naomba jalia.

wa ubani kumpata,iligharimu miaka,
 sana nilifurukuta,kila mkoa nasaka,
 hivi sasa nimepata,moyoni nimemuweka,
Maisha kuwa na mwenza,Mola naomba jalia.

 siku tulipoonana,tulikuwa safarini,
 sura yake kuiona,nilifurahi moyoni,
 ngozi mawaa haina,mfano ya utotoni,
Maisha kuwa na mwenza,Mola naomba jalia.

yeye hana majivuno,kwa kweli ni msikivu,
 ukutazama kiuno,na rangi yake angavu
 kwa kawaida maono,ni kama mtepetevu
Maisha kuwa na mwenza,Mola naomba jalia.

huyu niliyempata,kwa kweli sifa anazo,
 kama ni kwenye karata,kwa kweli garasha sizo,
 mizungu nitaikata,rahisi kama pulizo
Maisha kuwa na mwenza,Mola naomba jalia.

jina lake silitaji,naogopa wafitini,
 hilo ni sawa mtaji,ninalitunza sirini,
 kama ni utafutaji,sikuacha asilani
Maisha kuwa na mwenza,Mola naomba jalia.

No comments:

Post a Comment