Friday, September 2, 2011

KAZI NI KUPATA KAZI

Kichwani lanitatiza,swali lihusulo kazi,
kutwa kucha ninawaza,sijapata ufumbuzi,
majibu mengi nawaza,yote hayatoshelezi,
  Kweli huu ni ukweli,kazi ni kupata kazi.

Nilipokuwa shuleni,sana nilijiliwaza,
mitihani nikiwini,sana nitajiliwaza,
sikuwaza akilini,mambo yatanitatiza,
  Kweli huu ni ukweli,kazi in kupata kazi.

Nilipotafuta kazi,sana nilihangaika,
watu kunishuku wizi,kwa nilivyosakasaka,
rushwa kuiomba wazi,ofisini nikifika,
  Kweli huu ni ukweli,kazi ni kupata kazi.

Kazi nilipoipata,moyo ukanitulia
mapesa nitasakata,vijiweni watalia,
kumbe bado ni ukata,vibaya kusimulia,
 Kweli huu ni ukweli,kazi ni kupata kazi

Mshahara wasumbua,sivyo nilivyodhania,
sasa kilichobakia,siku kuzihesabia,
nashindwa kutegemea,lini watanipatia,
  Kweli huu ni ukweli,kazi ni kupata kazi..






















No comments:

Post a Comment