Friday, September 2, 2011

CHAKULA CHAKO WAKILA,HATA CHA MTOTO PIA!

Baba unanishangaza,unavyopenda chakula,
hakuna haja kuwaza,wala kumuomba Mola,
watoto unatukwaza,sasa twaanzisha vita,
  Chakula chako wakila,hata cha watoto pia

Watoto tukale wapi,ukila chakula chetu
watudanganya kwa pipi,pipi sio mila kwetu,
akili zetu si fupi,kutufanya ni vibutu,
  Chakula chako wakila,hata cha watoto pia

watoto twakushangaa,unavyodoea vyetu
chakula unanunua,tena kile cha kikwetu,
   vipi tena wachukua,hatupendi hiyo katu
  Chakula chako wakila,hata cha watoto pia.

Shilingi  mia kwa nini,wagombea na mtoto,
unapata milioni,tena njia za mkato,
kwa mtoto kuna nini,mambo yake batobato,
  Chakula chako wakila,hata cha mtoto pia.

Babu kaleta zawadi,nawe macho juu juu,
sijaiona abadi,tabia ya kijukuu,
kusema mi sina budi,sijepalia kifuu,
  Chakula chako wakila,hata cha mtoto pia.

Kile kilicho cha kwako,watoto hatukigusi,
vilivyo sirini mwako,waficha kama fukusi,
tunajua nia yako,mbaya mfano wa fisi,
  Chakula chako wakila,hata cha mtoto pia.

Nilipopewa mkate,wewe uliutamani,
ulianza meza mate,ukawaza akilini,
vipi ukaukamate,ukaufiche chumbani,
  Chakula chako wakila,hata cha watoto pia.

Vyakula vyako ni vingi,sote tunavibaini,
hatuviweki vigingi,wenda kula hotelini,
waweka gani misingi,tuliobaki nyumbani
  Chakula chako wakila,hata cha watoto pia.

















  






No comments:

Post a Comment