somo la umaridadi,wengi linatusumbua,
ninasema makusudi,tena nimekusudia,
kusema kwangu si budi,wote nitawaambia,
Umaridadi mzuri,ni kujali familia.
wengi twajipendekeza,tuonekanae kwa watu,
jinsi tunavyojikweza,kusema katu siwezi,
akili kuituliza,tokeni kwenye misitu,
Umaridadi mzuri,ni kujali familia.
wengine umaridadi,ni kuvaa suti safi,
chumbani wawashe udi,kuipata hewa safi,
watoto kwa makusudi,magodoro ni ya sufi,
Umaridadi mzuri,ni kujali familia.
kutwa unavaa tai,twakuona wapendeza,
wewe ni baba hufai,watu baki huwatunza,
nyumbani kwako hukai,watu baki wajikweza
Umaridadi mzuri,ni kujali familia.
michango mingi watoa,kila kamati hukosi,
majigambo wayatoa,kwa vikao vya harusi,
laki tatu unatoa,wewe huko ndiye bosi,
Umaridadi mzuri,ni kujali familia.
mama nawe washangaza,vitenge zamu kwa zamu
mtaani waongoza,watu imeisha hamu,
kanga nazo umejaza,watu wote twafahamu,
Umaridadi mzuri,ni kujali familia.
watoto nguo ni mbovu,mama atia huruma,
hebu uache uovu,baba jaribu kupima,
twaomba acha uovu,jaribu kuona nyuma,
Umaridadi mzuri,ni kujali familia.
mengi nimeyaongea,kuhusu umaridadi,,
haya sitawaonea,wafanyao makusudi,
huruma nawaonea,huo si umaridadi,
Umaridadi mzuri,ni kujali familia.
hapa mwisho nimefika,sana nimeongelea,
ujumbe ukikufika,ustarabu jongea,
sifa hovyo kujipaka,bure utaja umia
Umaridadi mzuri,ni kujali familia.
No comments:
Post a Comment