kupitia shairini,leo ninatoa zito,
lilokaa akilini,linanitia majuto,
jibu sijalibaini,moyo upate fukuto,
ndugu zangu mko wapi mbona barua sipati?
nikianza na walimu,shule msingi zamani,
walikuwa wakarimu,na roho zenye imani,
kunishikisha kalamu,kunitoa ujingani
ndugu zangu mko wapi mbona barua sipati?
Ndekwa ndiye wa awali,la kwanza alinifunza,
mwalimu Nzogya la pili,tebo ndiye alianza,
naye mama Mtawali,kingereza kunifunza,
ndugu zangu mko wapi mbona barua sipati?
sisahau marafiki,waliokuwa mahiri,
hakujua unafiki,Huseni Juma Omari,
Gene mtoto wa Laki,Mbeya kwenu nafikiri
ndugu zangu mko wapi mbona barua sipati?
Hezroni wa Ruyange,ukweli ulithamini,
kama safari nipange,nije kwako natamani,
hata kama ni Rulenge,nauli nitaiwini
ndugu zangu mko wapi mbona barua sipati?
moyoni nina shauku,nimuone Kachuchuru,
hata kama ni usiku,hakuutoa udhuru,
alikesha kila siku,kusikiza misururu,
ndugu zangu mko wapi mbona barua sipati?
siwezi kutaja wote,anuani yangu chini,
nitasafiri kokote,nikipata anuani,
maisha yapo popote,hapahapa duniani
ndugu zangu mko wapi mbona barua sipati?
Konisaga Mwafongo
0717248828;konisaga@yahoo.com
No comments:
Post a Comment