sisi sote wasafiri,safari yetu ni moja,
tulianza adhuhuri,kwa kuujenga umoja,
jambo tulilofikiri,tulifikiri pamoja,
Jahazi laenda kombo,naogopa tutazama.
kuivinjari bahari,unahitaji ujuzi,
nahodha awe mahiri,kuvikwepa vizuizi,
afikirie vizuri,tusipate pingamizi,
Jahazi laenda kombo,naogopa tutazama.
hata sisi wasafiri,busara tunahitaji
kazi iwe tafakari,na kumuomba mpaji,
tusiwe kama kafiri,tumuombe Muumbaji,
Jahazi laenda kombo,naogopa tutazama.
nahodha tunakuomba,safari iwe makini,
sio kwamba twajikomba,tukafike kisiwani,
wasafiri tunaomba,tuongoze kwa makini,
Jahazi laenda kombo,naogopa tutazama.
unahodha kazi ngumu,katu sitoiamini
kuliongoza vigumu,kundi ndani jahazini,
waweza pata wazimu,kama ng'ombe machinjoni,
Jahazi laenda kombo,naogopa tutazama.
wapi yu msaidizi,kupokea ukichoka,
tumepigwa bumbuazi,wenzetu watatucheka,
nahodha hukumaizi,mwenzio ana vibweka,
Jahazi laenda kombo,naogopa tutazama.
kitambo kimeshapita,bado hatujielewi,
njia ipi tumepita,mbona safari haiwi,
hatukuweza kupata,hata harufu ya Wawi,
Jahazi laenda kombo,naogopa tutazama.
dhoruba imetukumba,ubavu umetoboka
wewe bado unatamba,jahazi litaboreka,
abiria twakuomba,punguza vyako vibweka,
Jahazi laenda kombo,naogopa tutazama.
sasa nini tunafanya,kweli twaanza kuzama,
tunafanana na panya,anayehaha kuhama,
awali tulikukanya,sasa waanza lalama,
Jahazi laenda kombo,naogopa tutazama.
hapa mwisho nimefika,bado ninasononeka,
maafa yatatufika,hatuwezi nusurika,
mwisho hatutaufika,majini tutajizika,
Jahazi laenda kombo,naogopa tutazama.
No comments:
Post a Comment