Wednesday, September 14, 2011

ELIMU CHAI YA MOTO

Hapo kale tuliimba,elimu chai ya moto,
mashairi tulipamba,tuliyaimba kitoto,
mambo yaliyotukumba,leo hii kama ndoto
  Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie.

ukweli nimebaini,elimu kweli bahari,
kuandika vibaoni,hadi kwenye daftari,
unapofika shuleni,vingi unatahayari,
Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie.

waukumbuka umande,asubuhi na mapema,
wapata chai na kande,kasi huku ukihema,
gari wapi ukapande,wewe mtoto wa mama,
Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie.

hebu kumbuka walimu,walivyokuwa na wito,
asubuhi wajihimu,yale ni gani mapito,
hawakuwa warasimu,kufanya mambo mkato,
Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie.

wazikumbuka adhabu,zile walizozitoa,
zilikuwa na sababu,wala hawakukosea,
walitufunza adabu,na nidhamu kutopea,
Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie.

ulikuwa kama wimbo,lakini una maana,
haukuwa na mafumbo,wala beti kukinzana,
kichwani kama ulimbo,jinsi ulivyonatana,
Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie.

hebu kumbuka adhabu,kama kuchimba visiki,
ilikuwa kweli tabu,kama kuvunja kasiki,
yote yaliyonisibu,sasa yanipa riziki,
Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie

uji bila ya sukari,ilikuwa kawaida,
mfano sawa futari,bila asali si shida,
tebo tulivyokariri,kama mgonjwa na soda,
Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie.

ukifika sekondari,mambo yanabadilika,
sasa hakuna'habari',ung'eng'e kuutandika,
ilikuwa kweli heri,mambo yakaeleweka,
Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie.

huko elimu ya juu,mambo ni kizaazaa,
.hakuhitaji makuu,vingi utavishangaa,
hata walio wakuu,kule wengi wazubaa,
Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie.

ulichanganya'madesa',mambo yalipokutinga,
jambo lililokupasa,ni vizuri kujipanga,
 hilo sana sio kosa,bali ulipoboronga,
Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie.

umeingia kazini,huko hakuna kudesa,
ulichopata chuoni,kifanyie kazi sasa,
ulifanya'magirini',sasa wapata mikasa,
Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie.

elimu chai ya moto,ukinywa upulizie,
ni sawa kupata kito,nani akakutunzie,
elimu kweli ni moto,lazima upulizie,
Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie.

sasa ninamalizia,ELIMU kweli ni mali,
jinsi unavyodhania,pia tumia akili,
sio cheti fumbatia,kama ilivyo hamali,
Elimu chai ya moto,ukinywa upulizie.

No comments:

Post a Comment