Ndoa zetu siku hizi,ni kama tuko vitani,
ni rahisi kumaizi,vita huko majumbani,
huna haja kubarizi,ukweli kuubaini,
Ninazitamani ndoa,zile za mababu zetu.
Zimejaa fumanizi,ndoa kama ni utani,
nyingi ni za kipuuzi,linaniuma moyoni,
afadhali kikohozi,dawa hospitalini,
Ninazitamani ndoa,zile za mababu zetu.
Zilithamini makuzi,kweli nasema jamani,
koo zile zenye wezi,kuoa singetamani,
ndoa pasipo ujuzi,nani angezithamini,
Ninazitamani ndoa,zile za mababu zetu.
Sasa ndoa ni mapozi,yote haya naamini,
kama sio makohozi,ulotema mdomoni,
wote huu ni uchizi,linaniuma moyoni,
Ninazitamani ndoa,zile za mababu zetu.
Ndoa hii mwaka juzi,leo haina thamani,
nyumba sasa si makazi,ndani kutwa tafrani,
nani kwenu mchokozi,kasuluhisheni ndani,
Ninazitamani ndoa,zile za mababu zetu.
Ndoa sio mazoezi,kujaribu uwanjani,
likitokea dowezi,kwa mbali lifukuzeni,
muuache ubazazi,rudini ndani chumbani,
Ninazitamani ndoa,zile za mababu zetu.
Ndoa hizi siku hizi,hazimjui Manani,
kwa waganga kama kazi,hiyo kwenu kwenu ndio fani
Muumba hatumjuzi,tukigombana nyumbani,
Ninazitamani ndoa,zile za mababu zetu.
Namaliza kubarizi,ondokeni mkumboni,
msitumie hirizi,hamtodumu ndoani,
ndoa hizi za mizizi,jibu lake kaburini
Ninazitamani ndoa,zile za mababu zetu.
No comments:
Post a Comment