Nimejiuliza sana,wapi tunaelekea
kichwani ninajikuna,jibu kujitafutia
wakubwa wanatubana,haki yote yapotea,
Kazi walistaafu,tena mnawapa kazi.
Watoto twawasomesha,pesa nyingi tunalipa,
kutwa kucha walikesha,ile elimu kupata,
sasa mnawazungusha,tena sasa mwawatupa,
Kazi walistaafu,tena mnawapa kazi.
Nisemayo si majungu,ni jambo la uhakika,
imenitia uchungu,wanyonge twasikitika,
hata kule kwa wazungu ,jambo hili limefika,
Kazi walistaafu,tena mnawapa kazi
Hebu jaribu chunguza,haya ninayoyasema,
lakini kasi punguza,kazi yako iwe njema,
usije lengo poteza,ukabaki na kilema,
Kazi walistaafu,tena mnawapa kazi.
Udugu umeshamiri,ingawa tunaukana,
urafiki ni mahiri,wewe kando utabana
kazi sasa sio siri,mambo yote kujuana,
Kazi walistaafu,tena mnawapa kazi.
Mwasema ni wazoefu,ndio mana wanarudi,
yatia kichefuchefu,kusema sinayo budi,
sio maneno machafu,mimi nasema abadi,
Kazi walistaafu,tena mnawapa kazi.
Waliotoka shuleni,kazi waipate wapi?
mmejaa ofisini,wao wakauze pipi,
rejeeni vijijini,mmekuwa fotokopi,
Kazi walistaafu,tena mnawapa kazi.
Mtoto wa mkulima,ataishia kulima,
na hata akijituma,hapo kwenye taaluma,
mambo yalivyo mrama,ataishia lalama,
Kazi walistaafu,tena mnawapa kazi.
Elimu utayosoma,ikusaidie wewe,
usianze kuzozoma,ukajitia kiwewe
ninakukata kalima,kazi hizo za wenyewe
Kazi walistaafu,tena mnawapa kazi.
Mliopo makazini,kazi yenu ithamini,
wakiletwa ofisini,jamani wapokeeni,
lakini muwe makini,msingie matatani,
Kazi walistaafu,tena mnawapa kazi.
Beti hizo zinatosha,kama ukizingatia,
sio lengo kuwachosha,dukuduku nimetoa,
pumzi sasa nashusha,moyo unachekelea
Kazi walistaafu,tena mnawapa kazi.
No comments:
Post a Comment