Wednesday, September 14, 2011

TUWAHESHIMU WAZAZI

wazazi Mungu wa pili,hili sote twalijua,
lazima wawe wawili,katika hii dunia,
wanapoishi mahali,ni Mola kawajalia
  Tuwaheshimu wazazi,sana wamehangaika.

tulipokuwa wadogo,sana tulilalamika,
tulijifanya ni mbogo,chakula kihitajika,
hatukutaka muhogo,moyo haukuridhia,
  Tuwaheshimu wazazi,sana wamehangaika.

kulea kazi ya baba,hakika pia ya mama,
kuwalea kwa mahaba,ulezi si lelemama,
kama chakula ni haba,wazazi walijinyima,
Tuwaheshimu wazazi,sana wamehangaika.
walitupeleka shule,mambo mengi waliacha,
kwa pesa yao kichele,anasa waliziacha,
kwenda huku hata kule,walishindia mchicha,
Tuwaheshimu wazazi,sana wamehangaika.

uwezo waliopata,ndio waliotumia,
kidogo walichopata,ndicho walitupatia,
na pesa sio karata,dume ukajilambia,
Tuwaheshimu wazazi,sana wamehangaika.
kuwalaumu si haki,jaribu kufikiria,
hebu acha kuhamaki,maisha jifikiria,
tena uache dhihaki,wazazi luwarushia,
Tuwaheshimu wazazi,sana wamehangaika.

elimu waliyokupa,uitumie vizuri,
ulianza kaa hapa,maisha ukivinjari,
sasa nini unaapa,wazazi hawafikiri,
Tuwaheshimu wazazi,sana wamehangaika.

hivi sasa umeoa,una mkeo nyumbani,
ilani sasa watoa,huwataki asilani,
mahari waliyotoa,hukumbuki abadani,
Tuwaheshimu wazazi,sana wamehangaika

nitaongea mangapi,yote mbona mwaelewa,
busara nitoe wapi,wazazi wanaelewa,
mhariri toa kopi,watu wapate elewa,
Tuwaheshimu wazazi,sana wamehangaika.

No comments:

Post a Comment