Friday, September 2, 2011

USIWAIGE WAVUVI

Ziwani samaki wengi,wa aina mbalimbali,
wavuvi waona mengi,waweza usikubali
mitego mingi watega,mingine kwenye jabali,
  Wavuvi kazi wanayo,katu huwezi waiga

Wavuvi mahala pengi,hawavai suruali,
hawaibebi  mitungi,bali wana vibakuli,
mitego watega mingi,mingine kwenye jabali,
  .  Wavuvi kazi wanayo,katu huwezi waiga

Tembelea baharini,au wale wa ziwani,
kawaone wa mitoni,au kule mabwawani,
tofauti huioni,muda mwingi ni majini,
  Wavuvi kazi wanayo,katu huwezi waiga

Samaki aina nyingi,kuwapata ni adimu,
pweza ana visa vingi,aweza kutoa damu,
mbasa kwenye kina kingi,kumpata ni adimu,
 Wavuvi kazi wanayo,katu huwezi waiga.

Samaki niliyepata,wavuvi wanashangaa,
kozi hiyo sijapata ya kuingia kuvua,
samaki niliyepata,wote macho watumbua
  Wavuvi kazi wanayo,katu huwezi waiga

Nilipotupa ndoano,mshipi akaukata,
kitu nilichokiona,hasira ikanipata,
sikupenda kushindana,ujasiri nikapata,
 Wavuvi kazi wanayo,katu siwezi waiga.

Nikalitupa jarife,hili sasa litafaa,
hata ikibidi nife,samaki nitamvua,
hatalikata jarife,hivi nimeshamvua,
  Wavuvi kazi wanayo,katu siwezi waiga.

Samaki niliyevua,nitamtunza chumbani,
wengi mtanishangaa,simuweki sebuleni,
huyu kweli si dagaa,nimuanike juani,
  Wavuvi kazi wanayo,katu siwezi waiga.

Samaki kanisumbua,kutwa kucha kumtega,
kitu nilichogundua,hamkujua kutega,
muda ulipotimia,mtego hakuumega,
  Wavuvi kazi wanayo,katu siwezi waiga

Samaki ni mali yangu,sitogawana na mtu,.
namweka chumbani mwangu,katu hutoona kitu,
nitamfumbata mwangu,wamwone wazazi wetu,
 Wavuvi kazi wanayo,katu siwezi waiga. 










 









  











No comments:

Post a Comment