Tuesday, September 6, 2011

NYUMBA YA AJABU

Jambo hili lashangaza,kuanza kusimulia,
kutwa kucha ninawaza,niweze kuhadithia,
jambo hili lanikwaza,akili kutotulia,
  Kuishi ni kazi ngumu,mume na mke pamoja.

Mama anapokosea,hebu muite chumbani,
fidhuli wamletea,kubwatuka sebuleni,
busara ikitopea,nyumba yenu itawini,
  Kuishi ni kazi ngumu,mume na mke pamoja.

Mama anapokosea,wawaeleza watoto,
hekima imepungua,mambo ya mkato,
busara imepungua,mambo mfano pilato,
  Kuishi ni kazi ngumu,mume na mke pamoja

Mama kosa amefanya,umekwisha kasirika,
lini ulipomuonya,unaanza kubwatuka,
hata kama wamkanya,ameanza kirihika,
  Kuishi ni kazi ngumu,mume na mke pamoja

Mke nawe washangaza,linapotokea jambo,
unaanza kutangaza,na pengine kwa mafumbo,
sasa watakupuuza,yapunguze majigambo,
  Kuishi ni kazi ngumu,mume na mke pamoja

No comments:

Post a Comment