Tuesday, September 6, 2011
NGOMA
ngoma ina raha yake,ukijua mirindimo,
waume kwa wanawake,wote wanakuwa,
kupata utamu wake,hutouona ukomo,
Ngoma wapige ya kwao,kucheza tucheze yetu.
waipiga kinyakyusa,sisi tucheze kigogo,
utamu tutaukosa,hata walau kidogo,
hatutapata mikasa,nani kapata kisago,
Ngoma wapige ya kwao,kucheza tucheze yetu.
ngoma yenu yatukera,mnayotaka tucheze,
mwaipiga kwa papara,nani atuelekeze,
mnaimba mmefura,na makelele tupaze
Ngoma wapige ya kwao,kucheza tucheze yetu.
misamiati ya kwenu,sisi hatuielewi,
'sukari twanga kwa kinu'kaulize hat Wawi,
sasa mmebuni mbinu,kukatakata matawi,
Ngoma wapige ya kwao,kucheza tucheze yetu
lugha mnayotumia,mnapoanzisha wimbo,
mwaanza kwa kutulia,kumbe mbele mna mambo,
sisi hatukudhania,kumbe mna vijimambo,
Ngoma wapige ya kwao,kucheza tucheze yetu.
upembuzi yakinifu,wimbo huu umekifu,
mmejaza majisifu,machoni hamna hofu,
mjifunze kwa siafu,usawa sawa mkufu,
Ngoma wapige ya kwao,kucheza tucheze yetu.
hiyo yenu mikakati,imetuchosha jamani,
imepitwa na wakati,tokea zile zamani,
kama vipimo vya futi,wakati wa mkoloni
Ngoma wapige ya kwao,kucheza tucheze yetu
ngoma hiyo hatutaki,hatuwezi kuicheza,
uso tumepaka chaki,huko kando mwatubeza,
mmekuwa'mafataki'haki zetu mmemeza,.
Ngoma wapige ya kwao,kucheza tucheze yetu.
tuziache ngoma zao,nasi tucheze za kwetu,
tuviandike vibao,kueleza nia yetu,
hata vitabu vya Mao,tusome kwa nia yetu,
Ngoma wapige ya kwao,kucheza tucheze yetu.
kachague ngoma yako,uiimbe kwa lugha yako,
ya kwao sawa ukoko,hutocheza si ya kwako,
hata akilini mwako,imebaki sokomoko,
Ngoma wapige ya kwao,kucheza tucheze yetu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment