Tuesday, September 20, 2011

PENZI

umenipasha kwa wimbo,kwamba penzi walifuta,
kisa eti vijimambo,vingi ulivyovipata,
umenaswa na ulimbo,hunitaki katakata,
Huyo uliyemuona,ungeuliza ni nani.

ulitoka kwa vikumbo,mlango ulipopita,
na tena kwa majigambo,mabegi uliyavuta,
acha kufata mkumbo,mabaya yatakukuta,
Huyo uliyemuona,ungeuliza ni nani.

kwa ule wako urembo,mimi nilikufuata,
 wala sio kwa mapambo,yakanifanya kudata,
 kwangu wewe ndio nembo,moyoni imeninata,
Huyo uliyemuona,ungeuliza ni nani.
sitasema kwa mafumbo,penzi lako kulipata,
 moyoni unalo jambo,hakika lafurukuta,
 usiseme kwa mafumbo,vipi mimi takupata
Huyo uliyemuona,ungeuliza ni nani.

usiyarefushe mambo,huko kwenu nakufata,
 hata kama uko Mombo,mtwara hata Msata,
 penzi jamani ni fumbo,kamuulize Tilata,
Huyo uliyemuona,ungeuliza ni nani.

halitazami maumbo,penzi likikufuata,
 mashaibu kwa vifimbo,maajuza watafuta,
 halitizami muambo,popote litajikita
Huyo uliyemuona,ungeuliza ni nani.

No comments:

Post a Comment