Tuesday, September 6, 2011

KUOA KITU KIZURI,HATA KUOLEWA PIA

kuoa kitu kizuri,hata kuolewa pia,
kupata mke mzuri,hakika inavutia,
usioe wa kiburi,utakuja jijutia,
  Kuoa kitu kizuri,hata kuolewa pia.

hata wewe mwanamke,chagua mume makini,
usipate wa makeke,kamwe hatolala ndani,
kutwa mshikemshike,kutotulia nyumbani,
  Kuoa kitu kizuri,hata kuolewa pia.

huyo uliyechagua,umechagua vizuri,
sana uliangalia,akakutia kiwewe,
sasa nini unalia,suluhisheni wenyewe,
  Kuoa kitu kizuri,hata kuolewa pia.

mnapokorofishana,budi itaneni ndani,
ni lazima kupishana,na huyo wako mwandani,
kwa koo mmepishana,hata kwa ndani rohoni,
  Kuoa kitu  kizuri,hata kuolewa pia.

mara nyingi nashangaa,watu wanapogombana,
miaka mingi wamekaa,maisha yao mwanana,
watoto wamewazaa,tena wanaofanana,
  Kuoa kitu kizuri,hata kuolewa pia.

waume wanishangaza,msimamo wao duni,
siri zao watangaza,na mambo yao ya ndani
wameshindwa kuongoza,wanatanga mitaani,
  Kuoa kitu kizuri,hata kuolewa pia.

nawe mke wachekesha,jambo linapokufika,
usiku kucha wakesha,sana unahangaika,
usije moto kuwasha,maafa yatawafika,
   Kuoa kitu kizuri,hata kuolewa pia.

mambo yenu ya nyumbani,malizieni nyumbani,
si wazazi aslilani,katu hawatobaini,
kuwasumbua si shani,mtawapa tafrani,
  Kuoa kitu  kizuri,hata kuolewa pia.

mume mbio kwa wazazi,tatizo likitokea,
na mke bila ajizi,kwao enda simulia,
utafuteni mzizi,wa tatizo kutatua,
  Kuoa kitu  kizuri,hata kuolewa pia.

haya ni yangu mawazo,si jambo nasimulia,
isije leta mzozo,kwa walioyatukia,
ndoa mbovu ni uozo,hakika nawaambia
  Kuoa kitu  kizuri,hata kuolewa pia.

No comments:

Post a Comment