Friday, September 16, 2011

TUJENGE NYUMBA ZETU

upangaji kazi ngumu,hakika nimeamini,
nimeona umuhimu,niandike gazetini,
utakayosoma humu,nimeona kwa jirani,
  Ukijenga nyumba yako,hakika utatulia.

mijini tunamoishi,kuna mambo ya ajabu,
haihitaji ubishi,itakuja kupa tabu,
huwezi kamata moshi ,bure utajisulubu,
  Ukijenga nyumba yako,hakika utatulia.

kweli kodi tunalipa tena gharama ya juu,
 sio kwamba twajitapa,hatuyapendi makuu,
 umetukumba 'ukapa',neno hilo nanukuu,
  Ukijenga nyumba yako,hakika utatulia.

umeme bei wapanga,bila kuonyesha bili,
 kosa langu ni kupanga,huu ni mwaka wa pili,
 usidhani mi mchanga,nilipe elfu mbili,
  Ukijenga nyumba yako,hakika utatulia.

nikichelewa kidogo,geti tayari wafunga,
mimi sina nyumba ndogo,mbili siwezi kupanga,
sa' mbili muda mdogo,kazi zinaponitinga,
  Ukijenga nyumba yako,hakika utatulia.

siku moja nakumbuka,wiki moja ulinuna,
nini kilichokufika,hata salamu hakuna,
kumbe siku ilifika,mfukoni pesa huna,
  Ukijenga nyumba yako,hakika utatulia.

ukweli tabu twapata,sisi tusio na nyumba,
 shida zianpotupata,wao macho wanafumba,
 hawaujui ukata,wataka kodi ya nyumba,
  Ukijenga nyumba yako,hakika utatulia.

kulipa kodi ni haki,hiyo wote tunajua,
 chumba umenipa hiki,na jiko la kupikia,
 usinijengee chuki,kodi nitakupatia,
  Ukijenga nyumba yako,hakika utatulia.

nyumba yangu nikijenga,sana nitafurahia,
 vyumba nitavyovipanga,wengi mtatamania,
 nitakuacha kupanga,maisha kufurahia,
  Ukijenga nyumba yako,hakika utatulia.

tamati sasa nafika,pia namuomba mungu,
 na wakati ukifika,niijenge nyumba yangu,
 tabu zilizonifika,zinanitia uchungu,
  Ukijenga nyumba yako,hakika utatulia.

No comments:

Post a Comment