Tuesday, September 20, 2011

PESA WAPELEKA WAPI?

wengi watanishangaa,kuuliza swali hili,
wengine watazubaa,kuniita mswahili,
maswali yatazagaa,eti nifunge bakuli,
pesa wapeleka wapi,mbona mambo hayaendi?

nguo zako rapurapu,kwako viatu ni ndala,
wabugia taputapu,kwako imekuwa sala,
imebadilika shepu,kama nguruwe wa Ngwala,
pesa wapeleka wapi,mbona mambo hayaendi?

mkeo alalamika,hali nyumbani ni ngumu,
vitumbua anapika,kuupunguza ugumu,
kwenye pombe watukuka,nyumbani pesa ni ngumu,
pesa wapeleka wapi,mbona mambo hayaendi?

mumeo alalamika,kwamba haueleweki,
wapi unazipeleka,au chini ya kasiki,
wewe unajibweteka,mbona hauambilki,
pesa wapeleka wapi,mbona mambo hayaendi?

wazazi wajiuliza,hata ndugu zako pia,
umebaki kuwaliza,macho wanayatumbua,
sana umewachukiza,wapweke wamebakia,
pesa wapeleka wapi,mbona mambo hayaendi?

No comments:

Post a Comment