Hili wengi watacheka,nikianza simulia,
katu sifanyi vibweka,wazi nitaelezea,
mila zilivyotutoka,hatuna uasilia,
Nyingi si mila potofu,ni sisi tunapotoka.
Kwenye jambo la kuoa,wazazi walilijua,
sisi twajiamulia,wachumba jichagulia,
kule kwao hujajua,uchumba jitangazia,
Nyingi si mila potofu,ni sisi tunapotoka.
Huyo mke ulooa,wala kwao hupajui,
naye aliyekuoa,kesho atakukinai,
sababu usije zua,mila zao huzijui,
Nyingi si mila potofu,ni sisi tunapotoka
Magonjwa unayajua,kutaja yote siwezi,
zipo koo za vichaa,zingine za wadokozi,
lipi unaloshangaa,wengine ni wachochezi
Nyingi si mila potofu,ni sisi tunapotoka.
Lugha ile ya mafumbo,wazee walitumia,
hawakutumia fimbo,ujumbe kutupatia,
sasa vya nini vikumbo,tulia fuatilia,
Nyingi si mila potofu,ni sisi tunapotoka
Kwa mama wajawazito,kula mayai ni mwiko,
huu ulikuwa wito,kumbuka sayansi yako,
usiwaze kwa mkato,ulikuwa kweli mwiko,
Nyingi si mila potofu,ni sisi tunapotoka.
Zikumbuke enzi hizo,hospitali za shida,
kujifungua tatizo,tena kwachukua muda,
toto linene katizo,hili jibu sio mada,
Nyingi si mila potofu,ni sisi tunapotoka.
Hebu fanya uchunguzi,ndoa zile za zamani,
hawakuwa wapuuzi,wala ndani tafrani,
hizi ndoa siku hizi,ni kama tuko vitani
Nyingi si mila potofu,ni sisi tunapotoka.
Watoto wako wavivu,nini unachoshangaa,
umeshalipata kovu,katu huwezi litoa,
hata kama kwa mabavu,umeshaingia doa,
Nyingi si mila potofu,ni sisi tunapotoka
Beti kumi zinatosha,sasa nikapumzike,
hata kama zinachusha,ziweke mahali pake,
usasa umenichosha,ndoa zetu sekeseke
Nyingi si mila potofu,ni sisi tunapotoka.
No comments:
Post a Comment