Tuesday, September 6, 2011

NANI ATAKUTAFUTA

Mara nyingi nashangaa,kwa mambo ya walimwengu,
visa wanavyovizua,vinanitia uchungu,
majibu wanayotoa,yazua kizunguzungu,
  Nani atakutafuta,kama wewe ni fukara.

Kumbuka ulipofiwa,nani alikufuata,
ulibakia mkiwa,machozi kufutafuta,
hakuna ulichopewa,hata kande hukupata,
Nani atakutafuta,kama wewe ni fukara.

Kumbuka harusi yako,watu walivyokususa,
suti kama mbwa koko,au muuza msusa,
shela nalo ni kicheko,kama hukutoa pesa,
Nani atakutafuta,kama wewe ni fukara.

Kilio kimetokea,wewe hawakujulishi,
nini utajitolea,wanakuona mzushi,
machozi unayatoa,kwao sawa na bileshi,
  Nani atakutafuta,kama wewe ni fukara.

Busara kweli unayo,lakini pesa hauna,
hoja nzito utoayo,uzito kweli haina,
kazi yako ni miayo,kipara unakikuna,
 Nani atakutafuta, kama wewe ni fukara.

Kaka yako wa Kigoma,yeye anako kagari,
mdogo kule Dodoma,ana boma la fahari,
mdogo wako Satima,ana shamba la shayiri
Nani atakutafuta,kama wewe ni fukara


  

No comments:

Post a Comment