Wednesday, September 7, 2011

CHAKULANI WANISIMANGA.

kila atamani japo apate chakula,
njaa kweli si utani,kwa nini Mola kaumba,
sijaona asilani,kuishi bila ya kula,
Vipi unanisimanga,kula ulianza wewe.

uhai ni wa thamani,nawe pia unajua,
maisha sio samani,tuache mchwa bangua,
ukipata cha makini,afya utajijengea,
Vipi unanisimanga,kula ulianza wewe.

wasema nina tamaa,kisa ninataka kula,
uchu mimi umejaa,hiki ni chetu chakula,
simanzi imenikaa,ataniokoa Mola,
Vipi unanisimanga,kula ulianza wewe.

chakula kilipotengwa,ulivamia kwa pupa,
sasa imekuwa nongwa,nami hapo kujitupa,
ulafi ulivyosongwa,wala waacha mifupa,
  Vipi unanisimanga,kula ulianza wewe.

nakumbuka zama hizo,mimi bado kuzaliwa,
hukwenda hata likizo,ukitwange sawasawa,
uliyofanya uozo,katu hukusingiziwa,
Vipi unanisimanga,kula ulianza wewe.

unaniita mlafi,kisa nami nakitaka,
hata nipigwe makofi,sikubali nitafika
wewe kweli si msafi,wanawa kwa maji taka,
Vipi unanisimanga,kula ulianza wewe.

wanitangaza kwa watu,eti mimi vuvuzela,
nami sikubali katu,hapo wote tutakula,
hata nipigwe viatu,tutakutana mahala,
Vipi unanisimanga,kula ulianza wewe.

kila siku wala wewe,leo niachie mimi,
vipi wapata kiwewe,ulishapata uchumi,
wataka nipiga mawe,umekujaa umimi,
Vipi unanisimanga,kula ulianza wewe.

kichekesho umetoa eti sina uzoefu,
hebu nenda angalia,jinsi alivyo siafu,
jinsi anavyojitoa,tena moyo mkunjufu,
Vipi unanisimanga,kula ulianza wewe

muda wako umeisha,ulianza zama zile,
inakupasa kupisha,tena bila makelele,
chakula kimekutosha,na wana waache wale,
Vipi unanisimanga,kula ulianza wewe.

No comments:

Post a Comment