mwenzako anapotingwa,nini kinakuchekesha,
hata kama ni mfungwa,maombi yapasa kesha,
mwenzako anaponyongwa,nini chakufurahisha,
Hivyo vyote ni vicheko,mengine si ya kucheka.
pesa mfukoni hana,wewe unachekelea,
unaanza kumkana,kipi unafurahia,
una raha kumuona,kutwa akunyenyekea,
Hivyo vyote ni vicheko,mengine si ya kucheka
nimefeli mtihani,wewe unafurahia,
nimeshindwa kwenye fani,sherehe wajifanyia,
nimefukuzwa kazini,wasema uliyajua,
Hivyo vyote ni vicheko,mengine si ya kucheka
maombi bila majibu,yangu unachekelea,
kitu kipi cha ajabu,majibu ukisikia,
hiyo isiwe sababu,mimi nitasubiria,
Hivyo vyote ni vicheko,mengine si ya kucheka
mume wangu kanibwaga,wewe unachekelea,
kisa eti hakuaga,wadhani kanikimbia,
wahi nyumbani kuoga,fitina umezoea,
Hivyo vyote ni vicheko,mengine si ya kucheka
mke wangu kaondoka,wewe unafurahia,
machozi yakudondoka,vile ukichekelea,
ndoa yetu kuvunjika,wapweke tutabakia,
Hivyo vyote ni vicheko,mengine si ya kucheka
tukianza rudiana,wewe kwako ni msiba,
pembeni unajibana,majungu yako si haba,
amani kupatikana,japo katika kibaba,
Hivyo vyote ni vicheko,mengine si ya kucheka
kicheko kile halali,wewe kwako haucheki,
huzuni kila mahali,watu wote wakucheki,
furaha kwako muhali,umebaki kuhamaki,
Hivyo vyote ni vicheko,mengine si ya kucheka
cheka kicheko cha heri,tufurahi kwa pamoja,
sio kucheka pa shari,utavuruga umoja,
nakupasha kishairi,tazama hilo daraja,
Hivyo vyote ni vicheko,mengine si ya kucheka
beti kumi zinatosha,nyingi bure utachoka,
hayo niliyokupasha,moyoni hebu futika,
acha kujibabaisha,busara itakutoka,
Hivyo vyote ni vicheko,mengine si ya kucheka
No comments:
Post a Comment