ofisi hiyo si yako,umepewa ni dhamana,
mgeni kafika kwako,usimpime kwa dhana,
kumbuka yako miiko,sikiliza kwa mapana,
ewe bosi twakuomba,uwathamini wageni.
mgeni kafika kwako,wewe uko wimawima,
hajaja nyumbani kwako,kaja ofisi ya umma,
ofisi si chumba chako,ikumbuke yako dhima,
ewe bosi twakuomba,uwathamini wageni.
yupi utamthamini,aje amevaa suti,
au yule wa vimini,viatu kama mabuti,
siku utaja amini,kitumbua si chapati,
ewe bosi twakuomba,uwathamini wageni.
wageni wote ni sawa,bila kutazama hali,
sio kumjali Hawa,Konisaga hana mali,
Vita mwana wa Kawawa,Robert Msakamali,
ewe bosi twakuomba,uwathamini wageni.
No comments:
Post a Comment